Naitwa Khadija Abubakari Kauli, nilizaliwa tarehe 19 mwezi wa 4 miaka 23 iliyopita katika hospitali ya taifa ya muhimbili.
Kama nilivyotangulia kusema awali mimi nimezaliwa miaka 23 iliyopita nikiwa ni mtoto wa mwisho na pekee wa kike katika tumbo la mamangu, katika hali halisi tu hata kama ingalikuwa ni wewe hujawahi kupata mtoto wa kike au wa kiume ni dhahiri kuwa ungepatwa na furaha kubwa sana katika moyo wako si ndivyo? Hivyo ndivyo ilivyokuwa nafsi ya mamangu alipoambiwa amepata mtoto wa kike alifurahi sana na hakuamini mpaka pale aliponitia mikononi mwake, lakini furaha hiyo naweza sema iliingia doa nilipofikisha umri wa miezi mitatu tu baada ya kuanza kuumwa sana bila kujulikana kilichonisumbua, nilikuwa nikivimba mwili na mwili kubadilika rangi na kuwa ya njano lakini kwa kuwa mamangu alikuwa na uzoefu katika hilo japo hakuwa na uhakika ilibidi kunikimbiza hospitali ya taifa muhimbili bila kuchelewa kwa vipimo zaidi na ndipo hapo alipopatwa na huzuni baada ya kugundulika kuwa nina sickle cell anemia ugonjwa ambao nilirithi kutoka kwa baba na mama kwa maana wao wote walikuwa wana virusi vya ugonjwa huo, bila kuchelewa daktari aliamuru niachishwe ziwa la mama haraka iwezekanavyo ili kuzuia ugonjwa kusambaa zaidi na kuniweka katika matibabu ambapo kwa kuwa ugonjwa huo hauna tiba nilipewa dawa za kupunguza maumivu na dawa ziitwazo folic acid kwa ajili ya kuimarisha seli zangu ambapo tangu 1989 hadi leo 2012 bado natumia dawa hizo na itaendelea hivyo kwa maisha yangu yote hadi siku ntakayopumua pumzi yangu ya mwisho.
Nadhani mamangu alipatwa na uoga mkubwa na uchungu wa ndani kwa ndani kwa kuwa haikuwa mara ya kwanza kupata mtoto mwenye maradhi kama hayo aliwahi kupata mtoto wa kiume aliyeitwa Adamu mwenye maradhi kama yangu lakini baada ya miaka kadhaa baadae kabla ya kuzaliwa mimi alifariki dunia, hivyo kwa uhakika kila nilipoumwa mama yangu alipata uoga sana akijua atanipoteza muda wowote na saa yeyote, na kwa kuwa tangu nilipogundulika na ugonjwa nilikuwa ni mtu wa kukimbizwa hospitali kila mara baada ya hali yangu kuwa mbaya hasa usiku wa manane hivyo kwa kipindi hicho majirani wengi walikuwa wakishirikiana na mama kila alipohitaji msaada usiku wa manane na hata leo nikikutana nao huwa hawaamini kuwa ni mimi na swali la kwanza huwa we ndo khadija? Aisee kweli mungu mkubwa, ndo umekua hivyo, vp siku hizi huumwiumwi? Msalimie sana mama, na wengine hujikuta tu wakinisimulia wewe mtoto ulikuwa unamsumbua mamako sana kila mara ilitulazimu kukimbiza hospitali usiku wa manane kweli mungu mkubwa na mengine mengi.
Basi tangu hapo maisha yamekuwa magumu sana kwa upande wangu hasa baada ya kuanza shule na kutakiwa kujitegemea katika baadhi ya mambo yangu, maisha yangu karibu yote hasa wakati wa utoto nimeishi hospitali, kiukweli nimeishi maisha magumu sana sikuwa kama watoto wengine wa kawaida nilipenda iwe hivyo lakini kutokana na kuumwa mara kwa mara nilikosa haki zangu za msingi hasa kucheza na watoto wezangu kwanza binafsi niliathirika kisaikolojia kiasi cha kujiona kuwa mimi ni tofauti na wengine nikawa muda mwengine najitenga hasa nilipoanza maisha ya shule hususan shule ya msingi nilisoma shule ambayo tulikuwa tukichapwa sana lakini kulikuwa na sheria kuwa wagonjwa hawachapwi lakini unakuta mwalimu mwengine hajui hivyo ilinilazimu kuvaa alama nyekundu begani kiukweli hali ile was killing me sikupenda huwezi amini lakini hadi mstarini wagonjwa tulikuwa tukikaa kwenye mistari yetu wenyewe hatukutakiwa kujichanganya na wenzetu ile haikuwa nzuri na kama inaendelea nawashauri waache. Kila ijumaa kulikuwa na mchaka mchaka baada ya kutoka mstarini lakini sisi pia hatukuruhusiwa kukimbia sitopenda motto wangu aishi maisha niliyoishi mimi.
Lakini yote tisa kumi nilipoingia sekondari ambapo kwa uwezo wa mungu nilifaulu vizuri masomo yangu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wasichana jangwani mambo ndo yalipozidi kuwa magumu, mzunguko wa kuumwa uliongezeka zaidi na yote kwa yote nilikutana na mambo mapya, watu wapya ambao kwa namna moja ama nyingine ilikuwa lazima watambue hali yangu ili wajue jinsi ya kuishi na mimi, suala ambalo kwa kweli nilikuwa nikipata ugumu sana kuwaelezea watu na ni kitu ambacho huwa nakichukia hadi leo kwa kuwa hunikumbusha machungu mengi sana, nilipoanza fomu 1 siku moja mwalimu wa darasa aliingia kujitambulisha darasani akawa anapitia fomu ya kila mwanafunzi na ndo hapo alipopitia fomu yenye jina langu amabapo ilikuwa ni lazima uandike kama una maradhi yeyote nachokumbuka alichosema Yule mwalimu kilichonitoa machozi mbele ya darasa zima “khadija unaumwa sickle cell? Pole sana mwanangu mungu atakusaidia” nilijikuta tu nikilia kwani nilikumbuka jinsi ambavyo huwa naumwa na hapo darasa zima lilijua kuwa khadija anaumwa kitu ambacho pia huwa nakichukia katika maisha yangu, mpaka leo hii namkumbuka sana mwalimu Yule kwa kuwa baadae alikuja kuwa rafiki wa mama yangu baada ya siku moja kunipiga na kuumwa ilimbidi mama amfuate hadi shuleni lakini baadae walikuwa marafiki wakubwa baada ya kujikuta wakifanya kazi kwenye ofisi moja na hadi sasa huwa anakuja nyumbani.
Baada ya kuwa na ufahamu kuhusiana na hali yangu niliamua kuwa nataka nisome ili nije kuwa daktari nijitibu mwenyewe kama, na kama wengi wetu tujuavyo masomo ya sayansi huwa yanahitaji umakini mkubwa lakini kwa kuwa nilikuwa nikiumwa mara kwa mara na kulazwa mara nyingi nilijikuta nikiachwa nyuma kimasomo lakini kilichokuwa kikinisaidia ni kwa kuwa mungu alinipa akili za kuzaliwa zilizokuwa zikinisaidia katika masomo yangu na kunifanya nifanye vizuri mara kwa mara lakini hali ilibadilika nilipomaliza kidato cha pili na kusubiri matokeo, matokeo yalitoka na kwa bahati mbaya sikuwa nimefanya sana kwenye masomo ya sayansi hali iliyosababisha kuyeyusha ndoto zangu za kuwa daktari kwa maana ndo nilipeana mkono wa kwaheri na masomo ya sayansi, siku ile nililia sana kuona ndoto zangu zikiyeyuka mbele ya macho yangu pasi na kuwa na uwezo wa kufanya chochote nililia hadi nafika nyumbani na nilipofika tu nyumbani nilianza kuumwa , nilikata mwezi mzima nikiwa kitandani hali ilikuwa mbaya sana maumivu yalikuwa makali sana, lakini nilipopata tu nafuu kitu cha kwanza ilikuwa ni kukimbilia ofisini kwa mwalimu mkuu kuomba huku nikilia wanifikirie mara mbili kwani sikuwa tayari kuona ndoto zangu zikiyeyuka, jawabu nililojibiwa kwa kweli sitokaa nisahahu “we si unaunwa? Kwanini usisome masomo ya kawaida, sayansi huwezi kemikali zinakuathiri “niliganda kwanza moyoni nikajiuliza who are you to tell me what I can do n what I cannot do? Jambo ambalo pia nalichukia kuambiwa kuwa wewe huwezi kufanya kitu hiki kwasababu unaumwa. Niliumia sana sana kupita sana nikafikia hadi uamuzi wa kuhama shule lakini baadae nikasema hi indo njia ambayo mungu amaenichagulia siwezi jua kwanini nimepelekwa huku mungu ana makusudi na mimi wacha nisome. Nikaendelea na masomo yangu lakini pia nilikuwa na tabia ya ubishi kwani hata nilipokuwa naumwa bado nililazimisha kwenda shule nakumbuka siku moja hadi nilipoteza fahamu shuleni, wakati huo mama alikuwa njiani akielekea ofisini alipopigiwa simu alishuka haraka sana na kuchukua taxi kuja shule huku macho yamemjaa machozi akijua ananipoteza sasa, nilikimbizwa muhimbili kwa kuwa ndo ilikuwa hospitali ya karibu na baada ya kuwekwa mapumziko na kupatiwa matibabu madakatari walimshauri mama anipeleke nyumbani kutokana kuwa na hali yangu haikuwa vyema kuendelea kukaa pale ningeweza kuzoa maradhi mengine. Kwa kweli nilikuwa nikipenda zaidi kuwa mtu wa kawaida na kwa kuwa niliujua ukweli kuwa naumwa nilijitahidi kujiepusha na makosa ya hapa na pale na nashukuru mungu kwa namna moja ama nyingine nilifanikiwa.
Namshukuru mungu nilifanikiwa kumaliza kwa amani hadi kidato cha nne na matokeo yalipotoka yalikuwa mazuri na hivyo nilijiandaa kwa hatua nyingine as they always say “one step at a time” lakini katika hatua hii akili yangu ilikuwa na mpango mwengine kabisa ambao hata wazazi wangu hawakuwa wakifahamu nilikuwa nimedhamiria kubadili mazingira kabisa kwa kutaka kusoma boarding mkoa mwengine na hata katika uchaguzi wa shule nilioufanya sikuchagua hata shule moja ya jijini dare s salaam, nilichokuwa nakiwaza na kujiuliza ni kuwa “natakaa na wazazi hadi lini kwanini nisijaribu uzoefu mwengine wa maisha yap eke yangu, maisha mbali na wazazi haya ni maisha kuna leo na kesho sitokaa na wazazi siku zote naweza kuolewa siku moja na ukiacha kuolewa itakuaje kama kesho wakifumba macho nitakua mgeni wa nani? Nani atakubali kuishi na mimi katika hali hii? Inanilazimu kufanya hivi, ni lazima nijifunze kujihudumia mwenyewe mtiririko wa mawazo uliendelea kupita kichwani mwangu” ikabaki tu kusubiri uchaguzi wa shule utangazwe na kama nilivyodhamiria nilichaguliwa kujiunga na kidato cha sita katika shule ya sekondari morogoro maarufu kama moro sec mijini morogoro.kwangu binafsi nilifurahi kwa kuwa nilikuwa nimetimiza lengo langu lakini kwa wazazi wangu ilikuwa ni wasiwasi tele na mama alijaribu kunishawishi ili nikubali kufanya mpango wa kuhama shule lakini alikumbana na maswali ambayo hata yeye yalimfanya afikiri mara mbili na kwa shingo upande alikubaliana na maamuzi yangu nilimuuliza “mama leo mko hai sawa sisi ni wanadamu kuna leo na kesho, itakuaje mtakapofunga macho? Nitaishi na nani? Itanibidi nijifunze kuishi mwenyewe.”
Maandalizi yakaanza kwenda kuanza maisha mapya bila mama wala baba, japo nilikuwa na makaka kadhaa katika mji huo. Binafsi sikuwa na khofu hata kidogo kwani ni maisha niliyoyachagua mwenyewe na ni maamuzi yangu hivyo nilikuwa tayari kwa lolote, kama ungepata bahati ya kuchungulia begi langu hata kwa dakika ungeshangaa kwa kuwa lilisheheni madawa kuliko kitu chochote kile na makaratasi ya maelezo kutoka kwa daktari wangu juu ya dawa ninazotakiwa nizitumie na nisizotakiwa kutumia na maelezo yanayoelezea hali yangu kwa jumla na jinsi ninavyotakiwa niishi. Kwa siku za mwanzo maisha yalikuwa mepesi nay a kawaida lakini hali ilikuwa tete pale nilipoanza kuumwa nah ii ilitokana na kupata malaria mara kwa mara ugonjwa amabo ni adui yangu mkubwa na ndo ugonjwa ambao huamsha yote yaliyolala. Kwa kweli nilipoumwa nilipata tabu sanaaaa kwa kuwa kwanza ilikuwa ni lazima nilazwe hospitali ya mkoa kwa kuwa nilikuwa ni mwanafunzi wa shule ya serikali, na kama tujuavyo hospitali nyingi za serikali huwa na huduma mbovu na duni na kutokana na hali yangu nilihitaji uangalizi wa ziada hapo ndipo nilipokuwa nikikumbuka wazazi nyumbani nikatamani ningekuwepo nyumbani au hata mama yangu angekuwa karibu yangu, nilikatwazwa kulala na mtu yeyote marafiki zangu walikuwa wakifukuzwa na hivyo kulazimika kulala peke yangu, na nilipokuwa nikizidiwa na kulalama kwa maumivu usiku hakuna aliyekuwa akijali wala kushtuka sana sana labda unakuwa umewapatia la kuongea wakati wa kukabiziana zamu utawasikia “huyu ana ni sickler vikimzidia utamuona anajipinduapindua tu kitandani, kisha wote wanaangua vicheko” hizo ndo huduma za hospitali zetu za serikali. Vyoo pia vilikuwa vichafu mno mda mwengine hata maji hakuna hivyo kuoga ilikuwa ndoto za abunuasi, pili mara nyingi nilikuwa nikizidiwa usiku kama kawaida hivyo ilinibidi kuvumilia hadi asubuhi nap engine bado inapofika asubuhi matron akifuatwa atajibu anasali tumsubiri hadi amalize kusali ikiwa mimi naumia mana maumivu ya sickle cell huwa makali sana kiasi cha muda mwengine kupatwa na ganzi ya viungo hasa meno. Ilifika wakati mwengine ilimbidi mama kupanda gari hadi mororgoro kunichukua nyumbani kwa mmoja wa kaka zangu na kuniuguza hapo nipatapo nafuu ndo huondoka na kurejea ofisini hayo ndo maisha yangu nikiwa moro sec. wakati nikiwa kidato cha sita nilianza kuhisi hali tofauti katika mwili wangu hasa ilipofika saa usiku wa manane, nilihisi tumbo likiniwaka moto mara kwa mara niliamka na kuhangaika kutafuta chochote kitakachonipa nafuu baadae hali ilizidi ikanibidi nirudi nyumbani na baada ya vipimo nikagundulika kuwa na vidonda vya tumbo tatizo jengine likanipata. Kwa kweli hadi leo bado sijang’amua hali iliyosababisha kupata tatizo hilo lakini hadi sasa ninalo na huwa ninateseka mara mbili pale ninapoumwa.